Mama Afrika anawaita wanawe - 2015

(2015: Africa’s call to her children)

Wito huu nautoa kwa dhati ya moyo wangu
Wito uliodumu milele
Unaotokana na karne zilizokomaa kwa mateso
Karne za uvamizi na ubakaji wa uhuru na utu wetu
 
Mama Afrika anakwita wewe… ndio wewe…. na wewe tena
Anatuita sisi sote
Anatuambia: “Njooni”
Njooni enyi wanangu, njooni munikomboe
Msiniachie nikiteswa tena, nikinyonywa, nikidhalilishwa
Msiniache nikibakwa tena, nikishambuliwa
Msiniache nikikandamizwa, nikihongwa
Njooni mniokoe enyi wanangu
 
Nyinyi mlio karibu nami
Nyinyi mlio mbali kimwili lakini karibu kiroho
Nyinyi mliopotea katika mitaa baridi ya maadui
Nyinyi mpendao haki, mliosaliti, mlioasi
Nyinyi mliochoka, mliokonda, mlio wadhaifu, mnaotamani kulala
Amkeni, Amkeni
Nyanyukeni
 
SIMAMENI wima wanangu SIMAMENI!
Njooni kwenye chanzo changu cha ubinadamu
Njooni mjiimarishe katika mizizi yangu iliyokomaa
Njooni mpate nguvu mpya katika roho za mizimwi yangu
Njooni muoke joto kutoka moto wangu mtakatifu
Njoone mpumzike katika kivuli change chenye huruma
Mimi ni ardhi inayorutubisha, ardhi iliyo na rutuba ya kutosha
Matiti yangu ni machanga, maziwa yangu ni matamu
Mito yangu yanatiririka maji yanayopooza koo, yanayotuliza roho
Vito vyangu vinang’aa kutoka ardhini
Yote haya mtayarithi, kwa sababu nimewalea
Utajiri wangu ni mwingi licha ya uporaji
Utajiri wangu ni nguvu yenu adhimu licha ya utumwa
Utajiri wangu ni tabasamu yenu licha ya masaibu yote
Utajiri wangu ni roho zenu zinazopendeza licha ya majaribu yote
Nyinyi ni WANADAMU WENYE NGUVU
Mwishoni vaeni mpendeze
Kusanyeni nguvu zenu
Nawasubiri NYINYI, nimejaa matumaini kwa manufaa YETU sote
SIMAMENI wanangu, SIMAMENI na kateni minyororo
AMKENI AFRIKA, KILA MMOJA, KILA MMOJA, KWA PAMOJA, UBUNTU,
HATIMAYE TUMEUNGANA !!!!
---------------------------------------
Mtungaji Hulo Guillabert
Mkurugenzi wa Waafrika wa Diaspora
Mjumbe wa kamati ya Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Shirikisho la Umoja wa Afrika
(Mtafsiri Nizar Visram)